VIONGOZI WA KAUNTI YA POKOT WATAKA USALAMA KUIMARISHWA KAPEDO


Wakaazi wa kaunti hii ya Pokot Magharibi wakiongozwa na viongozi mbali mbali wa kisiasa wamejitokeza na kulaani vikali makabiliano ambayo yanaendelea kushuhudiwa katika eneo la Kapedo.
Wakiongozwa na mbunge wa Kacheliba Mark Lomunokal wakaazi hao wamesema kuwa itakuwa bora iwapo serikali kuu itaingilia kati ili kuhakikisha kwamba hilo linakomeshwa.
Akizungumza mjini Makutano Lomunokal hata hivyo ameirai serikali kutotumia nguvu kupita kiasi wanapoleta suluhu, kuumiza wananchi hasaa wa Tiaty.
Lomunokal hata hivyo ameilaumu serikali kwa kufeli kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha jamii ya Turkana na Pokot inalindwa.
Lomunokal kadhalika ameitaka serikali kutoa nafasi ya mazungumzo kufanyika baina ya kaunti hizo mbili.
Naye mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing amewashutumu vikali baadhi ya wabunge katika kaunti ya Turkana ambao walidai kuzingirwa na wezi wa mifugo wakitaka msaada wa kuondolewa eneo hilo, akisema kuwa viongozi hao wanaeneza uchochezi miongoni mwa wakazi.