VIONGOZI WA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAMEWAHAKIKISHIA WAKAAZI MCHUJO HURU NA WA HAKI.

Wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kujitokeza kuwaunga mkono wagombea nyadhifa mbali mbali za kisiasa wakati wa mchujo wa chama cha UDA.

Ni wito wake mgombea kiti cha ubunge eneo bunge la Kacheliba Ibrahim Long’olomoi ambaye aidha amewataka wakazi wa kaunti hii kuendelea kuunga mkono chama cha UDA anachokitaja kuwa chenye sera za kumnufaisha mwananchi wa hali ya chini.

Long’olomoi amesema kuwa wakazi wa kaunti hii walimpigia kura kinara wa chama cha ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu uliopita kama hatua ya kulalamikia oparesheni ya serikali eneo la bonde la kerio anayodai iliwadhulumu wakazi wengi, ila sasa wanamuunga mkono naibu rais William Ruto baada ya Raila kuamua kushirikiana na serikali.

Kando na hayo Long’olomoi amekosoa vikali oparesheni dhidi ya wahudumu wa boda boda ambayo hata hivyo ilisitishwa jana jumamosi akisema iliwadhulumu vijana wengi ambao hawana hatia kwa makosa yaliyotekelezwa na watu wachache akitaka serikali kuweka mikakati ya kuwasaidia vijana.