VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUSHIRIKI JUHUDI ZA KUAFIKIWA AMANI CHESOGON.
Viongozi wa dini katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuchangia katika juhudi za kuleta amani eneo la Chesogon mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama katika siku za hivi karibuni.
Akizungumza eneo la Kamaua eno bunge la Chepareria, mgombea kiti cha useneta katika kaunti hii kwenye uchaguzi mkuu wa mwakak ujao Julius Murgor amesema kuwa kanisa ni kiungo muhimu katika kuhakikisha amani ya nchi hivyo viongozi wa dini wanafaa kuhusika pakubwa katika swala hilo.
Murgor amesema kuwa hali ilivyo huenda shughuli muhimu eneo hilo zikaathirika pakubwa iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.
Murgor amesema kuwa licha ya vikao mbali mbali vya amani kuandaliwa eneo hilo bado kunashuhudiwa visa vya utovu wa usalama akitaka kutekelezwa maswala ambayo yanazungumziwa katika mikutano hiyo ili kutia kikomo kwa hali hiyo.
Kauli yake Murgor inajiri huku watu watatu wakiripotiwa kuuliwa kwa kupigwa risasi kufuatia makabiliano makali ya risasi yaliyotokea eneo hilo la Chesogon katika barabara kuu ya apolo kueleka chesogon kaunti hii ya pokot magharibi.
Akithibitisha kisa hicho OCPD wa marakwet mashariki Clement Mbavu amesema kuwa waliouliwa walikuwa katika pikipiki wakati waliposhambuliwa na genge hilo ambalo lilikuwa limejificha katika msitu ulio karibu.
Waliotekeleza mauaji hayo wanaaminika kutoka kaunti jirani na walikuwa na lengo la kulipiza kisasi.