VIONGOZI WA DINI WATAKA MAZUNGUMZO BAINA YA SERIKALI NA AZIMIO KUWAHUSU WAKENYA.
Viongozi wa kidini katika kaunti ya Pokot magharibi wameunga mkono mazungumzo baina ya serikali na chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya ambayo yananuia kutafuta mwafaka kuhusiana na maswala mbali mbali ambayo yamekuwa yakiibuliwa na upinzani.
Wakiongozwa na askofu wa kanisa la AIC kaunti hiyo David Kaseton, viongozi hao waliwataka wanachama wa pande zote mbili ambao wanahusika katika mazungumzo hayo, kuyachukulia kwa uzito kwa kuangazia maswala ambayo yanamhusu mwananchi na wala si kwa manufaa yao wenyewe.
Kaseton aliwataka wanachama hao kutokuwa na misimamo mikali wakati wa mazungumzo hayo kwa kuegemea mirengo yao ya kisiasa, bali waandae majadiliano hayo kwa nia moja ya kuhakikisha kwamba maswala ambayo yanawakabili wananchi yanapata suluhu.
“Mazungumzo ni muhimu sana iwapo tu lengo lake ni kuwafaidi wakenya wote. Wanachama wa pande zote mbili waendeleze mazungumzo hayo kwa nia ya kuangazia maswala ambayo yanamhusu mkenya wala si kwa malengo yao ya binafsi.” Alisema Kaseton.
Wakati uo huo Kaseton alitoa wito kwa wananchi kuzingatia ukomavu wa demokrasia na kuwa na mazoea ya kukubali matokeo ya chaguzi nchini, ili kuzuia mivutano ambayo imekuwa ikishuhudiwa kila baada ya uchaguzi kwani mengi ya mataifa kanda hii yanaitazama Kenya kuwa moja ya mataifa yaliyoendelea kidemokrasia.
“Tofauti za kisiasa zisiwe ni mazoea baada ya uchaguzi. Wakenya wanafaa kuwa na mazoea ya kukubali matokeo ya uchaguzi kwa sababu nchi nyingi ikiwemo majirani zetu wanaitazama Kenya kuwa moja ya nchi ambazo zimekomaa kidemokrasia.” Alisema.