VIONGOZI WA CHAMA CHA ODM WAMEJITOKEZA KUUNGA MKONO KAULI YA ODINGA KUHUSU SAJILI MBADALA YA WAPIGA KURA KUTUMIKA
Mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti hii ya Pokot magharibi Joseph Akaule ametetea hatua ya kinara wa muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga kushinikiza sajili mbadala ya wapiga kura kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti kando na ile ya kidijitali.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki muda mfupi uliopita, Akaule amesema kuwa kutumika sajili zote mbili kutahakikisha uwazi katika uchaguzi huo na kuzuia matukio ya chaguzi zilizotangulia ambapo mitambo hiyo ilifeli na kupelekea kile alichodai kuwa wizi wa kura.
Aidha Akaule ameisuta kauli ya mwaniaji urais wa chama cha UDA William Ruto kuwa hana tatizo hata iwapo tume ya uchaguzi IEBC ingesimamiwa na jamaa ya Raila, mradi kuwe na uwazi katika uchaguzi huo akimtaja kuwa mnafiki anayefahamu yaliyotukia katika chaguzi zilizotangulia.
Wakati uo huo Akaule amepuuzilia mbali madai ya Ruto na wandani wake kwamba idadi kubwa ya majina ya wapiga kura ambao ni wafuasi wake hasa kutoka ngome zake yamehamishwa katika sajili ya wapiga kura .