VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAWASUTA MAAFISA WA POLISI KWA KUWADHULUMU WANANCHI WANAPOENDESHA OPARESHENI YA KIUSALAMA.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuwasuta maafisa wa polisi ambao walivamia kijiji kimoja eneo la Lomut kwa kile walidai kuendeleza oparesheni ya kusaka silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria.

Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong na mwenzake wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao waliwasuta maafisa hao kwa kuwadhulumu baadhi ya vijana eneo hilo na kuwazuilia kwa madai ya kuwapata na silaha licha ya kwamba hamna silaha yoyote iliyopatikana wakati wa msako huo.

Viongozi hao sasa wamewataka maafisa wa usalama kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kukoma kuwadhulumu wananchi baada ya kushindwa kuwakabili wahalifu wanaowahangaisha wakazi wa maeneo hayo ya mipakani.

“Tunaambiwa kwamba kuna vijana ambao walipatikana eneo la Lomut na silaha katika msako ambao uliendeshwa eneo hilo. Tunashangaa kwamba polisi waliamua kuwawekelea vijana hao makosa ambayo hawakuhusika. Tunataka maafisa hao wafanye kazi kwa ukweli. Si kuanza kuwanyanyasa wananchi kwa kushindwa kutekeleza kazi yao.” Walisema.

Viongozi hao aidha waliitaka idara ya usalama kuwashughulikia vijana waliodhulumiwa  kwa kuhakikisha kwamba wanapata matibabu kufuatia majeraha walioyopata mikononi mwa maafisa wa polisi, wakitaka maafisa waliohusika uovu huo kuchukuliwa hatua ili wahusika wapate haki.

“Tunataka idara ya usalama kuhakikisha kwamba hawa vijana ambao walidhulumiwa na polisi wanapelekwa hospitali na kutibiwa. Hawa polisi waliofanya unyama huu pia wanapasa kuchukuliwa hatua ili waliodhulumiwa wapate haki.” Walisema.