VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATISHIA KUISHITAKI UINGEREZA KUFUATIA DHULUMA DHIDI YA WAKAZI ENZI ZA UKOLONI.
Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametishia kuishitaki serikali ya uingereza kwenye mahakama ya kimataifa kufuatia dhuluma zilizoendelezwa na serikali hiyo kwa jamii ya Pokot wakati wa vita vya ukombozi wa taifa hasa kwa wafuasi wa dhehebu la dini ya mafuta pole africa.
Wakizungumza eneo la Keringet kwenye sherehe ya ukumbusho wa mwanzilishi wa dhehebu hilo Lukas Pkiech, viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto wametaka wafuasi wa dhehebu hilo walioathirika zaidi kufidiwa na serikali ya uingereza.
Viongozi hao wamesema kuwa wakazi wengi katika kaunti hii akiwemo mwanzilishi wa dhehebu hilo waliteswa na kuuliwa kinyama na wakoloni.
Viongozi hao aidha wamesema mauaji ya halaiki katika eneo la Kolowa yaliyotekelezwa na wanajeshi wa uingereza, yalipelekea zaidi ya watu 400 hasa wafuasi wa dhehebu hilo kupoteza maisha yao wakisisitiza ni lazima serikali ya uingereza iwajibishwe.