VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KWA MANUFAA YA WAKAZI.

Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ametoa wito kwa viongozi katika kaunti hiyo kushirikiana na kuweka maslahi ya wakazi mbele ili kuhakikisha kwamba wananufaika pakubwa chini ya uongozi wa sasa.

Poghisio ambaye pia alikuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti alisema ni jukumu la uongozi wa sasa kuhakikisha kwamba wananchi wa kaunti hiyo wananufaika kutokana na miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa.

Alisema kuwa ipo haja ya fedha ambazo zinaletwa chini ya serikali za magatuzi kusalia kwenye kaunti hiyo ili kuimarisha uchumi wa wakazi, kwa kuhakikisha kwamba kandarasi zote zinazotoilewa kwa miradi mbali mbali, zinatolewa kwa wafanyibiashara ambao ni wenyeji.

“Viongozi wetu washirikiane, waweke maslahi ya wakazi mbele kwa kufanya kazi kwa pamoja. Hii miradi ambayo inatekelezwa hapa inafaa kuwanufaisha wakazi wa kaunti hii. Kandarasi zote zinazotolewa ziwaendee wakazi wa hapa. Pesa hazifai kutoka kaunti hii zikienda nje.” Alisema Poghisio.

Wakati uo huo Poghisio alitoa wito kwa wataalam mbali mbali kutoka kaunti hiyo kutoa ushauri kwa uongozi na hata kukosoa panapostahili ili kuhakikisha kwamba kaunti hiyo inaelekea panapostahili kwa manufaa ya mwananchi.

“Wataalam wote kutoka kaunti hii hata wale ambao wako nje ya kaunti lakini ni wazawa wa Pokot magharibi wanapasa kuwa na kitu cha kusema kuhusu uongozi wa sasa. Wakosoe panapostahili na kutoa mwelekeo ili kusaidia serikali kuhudumia wananchi inavyopasa.” Alisema.