VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA VITUO VYA POLISI KUJENGWA KWA WIKI MAENEO YA MIPAKANI ILI KUIMARISHA DORIA ZA KIUSALAMA.

Aliyekuwa mwakilishi wadi maalum kaunti ya Pokot magharibi Grace Rengei ametoa wito kwa serikali kujenga vituo vya polisi maeneo ya mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani za Baringo, Elgeyo Marakwet na Turkana.

Rengei alisema kwamba utovu wa usalama umekithiri pakubwa maeneo hayo kutokana na hali kwamba hamna kituo cha polisi hata kimoja hali inayowapa nafasi wahalifu kutekeleza uvamizi dhidi ya wakazi  hadharani bila ya wasiwasi wowote.

Akizungumza na kituo hiki Rengei alisema kwamba ni jukumu la serikali kisheria kuhakikisha usalama wa wananchi wake pamoja na mali yao, akiongeza kwamba jukumu hilo halipasi kuachiwa tu maafisa wa akiba NPR, bali watangamane na maafisa wa polisi.

“Tunaomba kwa haraka kwamba vituo vya polisi vijengwe maeneo ya mipakani pa kaunti hii na kaunti jirani za Baringo, Turkana na Elgeyo Marakwet. Kwa sababu ni jukumu la serikali kuhakikisha usalama wa wananchi na mali yao. Wasilete tu maafisa wa NPR.” Alisema Rengei.

Wakati uo huo Rengei aliitaka serikali kufungua maeneo hayo kwa kujenga barabara za kiusalama ili kufanya rahisi kwa maafisa wa polisi kuendesha doria na kuimarisha usalama wa wakazi, kwani kwa sasa hamna barabara za kutegemewa maeneo husika.

“Barabara za maeneo haya zinapasa kujengwa ili kuwarahisishia maafisa wa polisi kuendesha doria na kuwahakikishia wakazi usalama. Kwa sasa hakuna barabara nzuri ambazo magari ya polisi yanaweza kupitia maeneo haya.” Alisema.