VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA USAWA KATIKA OPARESHENI YA KUWAKABILI WAHALIFU BONDE LA KERIO.

Mbunge wa pokot kusini David Pkosing ameendeleza shinikizo kwa waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuwaajiri maafisa wa akiba NPR katika kaunti ya Pokot magharibi ili kusaidia katika kuimarisha usalama hasa maeneo ya mipakani.

Akizungumza katika hafla moja eneo la Kamelei huko Tapach, Pkosing alisema kwamba japo haungi mkono matumizi ya maafisa wa NPR katika opresheni ya kukabili wahalifu, ni vyema kuwepo na usawa hasa baada ya maafisa hao kuajiriwa katika kaunti jirani.

Aidha Pkosing alitaka maafisa wa NPR waliokabidhiwa bunduki katika kaunti jirani kupokonywa bunduki hizo baada ya madai kuibuka kwamba huenda silaha zinazotumika na wahalifu kuendeleza visa vya uvamizi ni za maafisa hao.

“Hili swala la NPR nilikuwa nakataa. Lakini kwa sababu majirani zetu wako nao na wanawasaidia kidogo, lazima kuwe na usawa ili twende pamoja. Lakini sasa zile bunduki ambazo maafisa wa NPR katika majirani zetu walipewa zinafaa kurejeshwa ili tuwe na usalama eneo hili.” Alisema Pkosing.

Wakati uo huo Pkosing alipuuzilia mbali madai kwamba amekuwa akiwafadhili washukiwa wa wizi wa mifugo ambao wamekuwa wakisababisha utovu wa usalama, akiyataja madai hayo kuwa porojo za kisiasa ambazo zinaenezwa na wapinzani wake wa kisiasa.

“Waziri Kindiki alikuja eneo hili na baada ya kutoka, watu wakauliwa. Mimi nikaja huku wakati mwingine nikitaka kujenga kambi ya polisi, nikaambiwa haijawekwa kwenye gazeti rasmi la serikali. Lakini nilipotoka siku iliyofuata watu wakauliwa. Sasa propaganda zikaanza kuenezwa na wapinzani wangu wa kisiasa kwamba mimi nafadhili wahalifu. Hawa ni watu wa kutaka tu kuniharibia sifa.” Alisema.