VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA SHULE ZA MIPAKANI KUPEWA KIPAU MBELE KWA MGAO WA BASARI.

Na Benson Aswani.

Viongozi wa maeneo ya mipakani katika kaunti ya Pokot magharibi ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama wametoa wito kwa gavana wa kaunti Simon Kachapin kutoa fedha za kutosha za basari kwa shule za maeneo hayo.

Wakizungumza katika hafla moja eneo la Chester, viongozi hao walisema kwamba serikali ya kaunti hiyo inapasa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wanafunzi katika shule za maeneo yasiyo salama hawatumwi nyumbani kila mara kutafuta karo bali wasalie shuleni  ambako kulingana nao ndiko kuliko na usalama.

Aidha viongozi hao wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Weiwei David Moiben, walisema juhudi zote zinapaswa kuelekezwa kwa shule hizo ikizingatiwa kwamba huathirika zaidi kutokana na harakati za wahalifu ambao wanaendeleza wizi wa mifugo.

“Shule ambazo zinapatikana maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama zinapasa kupewa kipau mbele katika utoaji wa fedha za basari kwa shule. Hii itasaidia kwa wanafunzi kusalia shuleni na kuzuia hatari ya kuvamiwa na wahalifu wanapotumwa nyumbani kwa ajili ya karo.” Moiben.

Viongozi hao aidha wamewataka wabunge kwenye bunge la kitaifa kutoka kaunti hiyo ya Pokot magharibi  kushinikiza kutengwa fedha za kuimarisha hali ya chuo kikuu cha walimu cha Chester ikizingatiwa ndicho chuo pekee kinachopatikana eneo hilo.

“Nawaomba viongozi wetu wabunge katika bunge la kitaifa kwamba washinikize fedha zaidi za kuimarisha hali ya chuo cha walimu cha Chester, kwa sababu hiki ndicho chuo pekee ambacho kinapatikana eneo hili.” Alisema.