VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA SHUGHULI ZA KENGEN KUREJESHWA TURKWEL.


Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameisuta serikali kwa kile wamesema kwamba imehamisha shughuli za kampuni ya KenGen hadi mjini Kitale kaunti ya Trans nzoia.
Wakiongozwa na mbunge wa Kacheliba Titus Lotee viongozi hao walisema hatua ya kuhamisha shughuli hizo kutoka Turkwel kwa kisingizo cha utovu wa usalama ni kuidhalilisha jamii ya kaunti hiyo.
Alisema wakazi wengi waliokuwa wameajiria kuhudumu katika kampuni hiyo walipoteza ajira kufuatia hatua ya kuhamishwa shughuli zake hadi mjini Kitale.
“Kampuni ya KenGen ilipoanza kulikuwa na utovu wa usalama, ila kampuni hiyo ilitekeleza mengi ikiwemo kuwaajiri wakazi wengi ila kutokana na sera ambazo hazina msingi, shughuli za kampuni hiyo zilihamishwa hadi mjini Kitale. Hatua hii ni kukandamiza jamii ya Pokot.” Alisema Lotee.
Lotee sasa anataka shughuli za kampuni hiyo kurejeshwa katika kaunti ya Pokot magharibi ili kuwanufaisha wakazi wa kaunti hiyo.
“Kama mbunge wa eneo hili nataka serikali ya rais William Ruto na kaimu afisa mkuu wa KenGen warejeshe huduma za kampuni hiyo eneo la Turkwel ili wakazi wa kaunti hii wanufaike na huduma zake.” Alisema.