VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATAKA KOMBE LA MURKOMEN KUSITISHWA KWA KUKOSA KUAFIKIA MALENGO YA KULETA AMANI.
Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi sasa wanataka mashindano ya kombe la Murkomen, kusitishwa mara moja kwa kile wamedai kwamba yamekosa kuafikia malengo ya kuhakikisha amani katika kaunti hiyo.
Wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Sook ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo Martine Komongiro, viongozi hao walisema kwamba hapana haja ya mashindano hayo kuendelea wakati ambapo wakazi wamezidi kuuliwa kiholela, baadhi wanaosababisha hali ya utovu wa usalama wakidaiwa kuwa maafisa wa serikali.
Komongiro alisema ni vyema kipute hicho kusitishwa kwa muda hadi patakaposhuhudiwa amani hasa maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo.
“Sisi kama viongozi katika kaunti hii tunataka mashindano ya kombel la Murkomen kusimamishwa mara moja. Kwa sababu mashindano haya yalianzishwa kwa lengo la kuleta amani eneo hili ila sasa hali imezidi kuwa mbaya zaidi. Ingawa malengo yake yalikuwa mazuri lakini yamefeli kuyatimiza.” Alisema Komong’iro.
Alimtaka mdhamini wa mashindano hayo waziri wa barabara Kipchumba Murkomen kuiga mikakati iliyowekwa na balozi Tegla Lorupe alipoandaa mashindano ya riadha kwa lengo la kuleta amani na ambayo yaliafikia malengo.
“Namwambia rafiki yangu Murkomen kwamba, anafaa kuiga mikakati iliyowekwa na balozi Tegla Lorupe wakati akiandaa mbio za marathon kwa lengo la kudumisha amani na ambalo liliafikia malengo yake.” Alisema.