VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WASISITIZA HAJA YA KUPEWA KIPAU MBELE WAKAZI KATIKA ZOEZI LA USAJILI WA WALIMU.


Viongozi mbali mbali wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuishinikiza tume ya huduma kwa walimu TSC kuhakikisha kwamba wanatendea haki wakazi wa kaunti hiyo kwa kuwapa kipau mbele katika shughuli ya kuwaajiri walimu inayoendelea.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alisema kwamba ni sharti nafasi zote 21 za walimu wa msingi na 119 wa shule za upili ambazo zimetengewa eneo hilo ziendee wakazi wa eneo hilo.
Lochakapong alisema kwamba kama viongozi wamejitolea kuhakikisha kwamba wakati huu wakazi wa kaunti hiyo wanapokea huduma ambazo wanastahili na zilizo sawa na maeneo mengine ya nchi.
“Eneo la Pokot ya kati tulipewa nafasi 21 za walimu wa shule za msingi na 119 za walimu wa shule za upili. Kile naiambia tume ya walimu TSC ni kwamba wawatendee haki wakazi wa pokot ya kati ili hizi nafasi zote ziwaendee wakazi wa eneo hili.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong alisema kwamba kwa ushirikiano na viongozi wengine eneo hilo la Pokot ya kati watafuatilia kwa karibu zoezi hilo kuhakikisha kwamba linaendeshwa kwa njia ya haki kuhakikisha wanaonufaika ni wakazi wa eneo hilo na si watu kutoka maeneo mengine.
“Tumeelewana viongozi wote wa eneo hili kushirikiana kuhakikisha kwamba wakazi wa eneo hili wanapata haki yao. Tumekubaliana kufuatilia zoezi hili hadi mwisho ili wakazi wetu wanufaike kwa kupewa nafasi ambazo wanastahili.” Alisema.