VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WASHUTUMU VISA VYA MIOTO SHULENI.
Na Benson Aswani
Viongozi kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kukashifu kukithiri visa vya kuteketezwa majengo ya shule ambavyo vimeonekana kukithiri katika siku za hivi karibuni nchini.
Wakiongozwa na mwakilishi kina mama katika kaunti hii Lilian Tomitom, viongozi hao wametoa wito kwa wadau mbali mbali ikiwemo walimu na wazazi kushirikiana katika kuweka mikakati ya kuzuia visa hivi kwa kuangazia kwa karibu mienendo ya wanao.
Aidha Tomitom amewataka viongozi wa kisiasa pia kushirikiana na walimu katika kusuluhisha baadhi ya maswala ambayo huenda yanachagia mikasa ya mioto ikiwemo kuimarisha miundo msingi huku akiwashauri wanafunzi kuzingatia masomo yao na kuepuka utovu wa nidhamu.
Kwa upande wake mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ameunga mkono hatua ya kuwapa wanafunzi likizo fupi kama njia moja ya kukabili visa hivi japo akisema kuwa isiwe lazima kwa kila mwanafunzi kwani wapo wanafunzi ambao wanatoka mbali ikizingatiwa siku chache ambazo wametengewa likizo hiyo.