VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WASHUTUMU MBINU ZINATOTUMIKA KUKABILI UTOVU WA USALAMA BONDE LA KERIO.


Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin aliongoza viongozi katika kaunti hiyo kushutumu serikali kwa kile walidai kuihami jamii moja kwa silaha katika kukabili utovu wa usalama kwenye kaunti za bonde la kerio na kuzitenga jamii zingine.
Wakizungumza katika mkutano wa amani eneo la Arpolo Chesogon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet, viongozi hao walisema kuwa hatua hiyo ni ishara kwamba serikali imefeli katika majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa wananchi.
Walisema hali hiyo imechangia taharuki miongoni mwa wakazi wa maeneo ya mipakani pa kaunti hizi mbili.
“Sisi kama viongozi wa Pokot tunapinga vikali kupewa silaha wananchi wa jamii moja. Ukiona serikali inapatia wananchi silaha ni thibitisho kwamba imefeli katika jukumu lake la kuweka usalama. Kuhami jamii moja kumechangia taharuki maeneo haya.” Alisema Kachapin.
Viongozi hao walimsuta vikali waziri wa usalama wa ndani ya nchi Kithure Kindiki wakisema kwamba anatekeleza majukumu yake kwa mapendeleo na kwamba ataandikisha historia kuwa waziri aliyefeli pakubwa katika huduma zake kwa wananchi.
“Kindiki ataandikisha historia ya kuwa kiongozi ambaye amefeli kabisa katika majukumu yake. Yeye anafanya kazi kwa kupendelea jamii moja huku jamii zingine eneo hili zikiendelea kuhangaishwa na wahalifu.” Walisema.
Kwa upande wake naibu kamishina eneo la pokot ya kati jeremiah Tumo alilalamikia ukosefu wa magari kwa maafisa wa polisi eneo hilo hali inayofanya vigumu kwao kuendeleza doria inavyohitajika, akiomba pia kufunguliwa barabara kadhaa eneo hilo kurahisisha shughuli zao.
“Tunakabiliwa na wakati mgumu kuendeleza doria maeneo ya huku kutokana na ukosefu wa magari ya usalama. Tunaomba pia barabara sita za eneo hili kufunguliwa ili kufanya rahisi kwetu kwendeleza doria.” Alisema Tumo.
Wakazi wa eneo hilo waliitaka serikali kufanya juhudi za kutia kikomo kwa swala la utovu wa usalama wakisema kwamba wamepitia hali ngumu kwa kipindi kirefu.