VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAPUUZA KUZINDULIWA CHAMA CHA KUP.

Na Benson Aswani
Viongozi mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kupuuza hatua ya kuzinduliwa chama kipya katika kaunti hii.
Wa hivi punde kutolea hisia hatua hiyo ni seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio ambaye amewataka wakazi kutohadaiwa na kile amedai vyama vya kikabila vinavyobuniwa bila kuwahusisha watu wengine na badala yake kuunga mkono vyama vitakavyohakikisha wanapata sauti ya kuamua hatima ya uongozi wa taifa.
Poghisio amedai kuwa wahasisi wa chama hicho gavana John Lonyangapuo na mbunge wa Pokot kusini David Pkosing wanatumia fursa hiyo kufuja fedha za umma ambazo zilifaa kutumika kuendeleza miradi ya kuwanufaisha wakazi wa kaunti hii.
Wakati uo huo Poghisio ametoa wito kwa viongozi wengine kaunti hii kuungana ili kubuni serikali itakayohakikisha mkazi wa kaunti hii anapata huduma zinazostahili na kuondoa uongozi ambao kulingana naye umeendelea kuwanyanyasa wakazi.