Viongozi pokot magharibi waomboleza watu wanne walioangamia katika ajali, Uganda

Gari lililohusika Kwenye ajali Tapaach, Picha/Maktaba
Na Benson Aswani,
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuomboleza vifo vya watu wanne, walioangamia kufuatia ajali mbaya ya barabarani jumamosi usiku kwenye eneo la Tapaach, barabara ya moroto kuelekea loroo nchini uganda.
Wanne hao ni pamoja na philemon lotudo, elijah lopuke, jackson kariwoi na ben Plimo.
Akiongoza viongozi wengine kaunti hiyo kuomboleza vifo vya nne hao, Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin aliwataja kuwa wachapakazi, waadilifu na wazalendo kwa wakazi na kaunti ya pokot magharibi.
“Nasikitika sana kufuatia taarifa za kufariki wenzetu wanne waliokuwa wakirejea kutoka taifa jirani la Uganda. Walikuwa viongozi ambao walijitolea kuwahudumia wakazi wa kaunti hii, na kuaga kwao ni pigo sana kwetu,” alisema Gavana Kachapin.
Hata hivyo kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo martin komongiro, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya moi jijini eldoret kaunti ya uasin gishu baada ya kunusurika.
Aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo ya pokot magharibi Samwel Poghisio katika risala zake aliwataja waliopoteza maisha kuwa maafisa shupavu, na walioonyesha nia ya kuwahudumia wakazi wa pokot magharibi.
Dkt poghisio aliwataka Wakazi wa kaunti hiyo ya pokot magharibi kuwa watulivu msimu huu wa maombolezo.
“Tunasikitika Sana kuwapoteza watu ambao walikuwa wamejitolea kuwahudumia na kuhakikisha maisha bora kwa wakazi wa kaunti hii. Naomba Mungu awape nguvu jamii za waliopoteza wapendwa wao wakati huu mgumu,” alisema Poghisio.
Mbunge wa Sigor Peter lochakapong pia ni miongoni mwa viongozi ambao wamewaomboleza waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo.

“Ni huzuni kubwa kwa ajali ambayo ilitokea katika taifa jirani la Uganda na kuwahusisha baadhi ya viongozi wetu ambao walipoteza maisha. Nasema pole kwa jamii na marafiki wa wale waliopoteza maisha,” alisema.
Kuhusu watumiaji wa mitandao ya kijamii, lochakapong aliwaonya dhidi ya kuchapisha jumbe za kupotosha na kutia wasiwasi, huku akiwataka wakazi na viongozi kutoelekeza kidole cha lawama kwa yeyote kutokana na ajali hiyo, badala yake kuungana na kuomba kwa ajili ya waliowapoteza wapendwa wao.