VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WALAUMIWA KWA KUENDELEZA SIASA BADALA YA KUWAHUDUMIA WANANCHI.

Wito umetolewa kwa viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi kushirikiana kikamilifu na kuwahudumia wananchi licha ya tofauti ya vyama vyao vya kisiasa.

Aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo John Lonyangapuo aliwasuta baadhi ya viongozi ambao alisema wameanza kuendeleza maswala ya siasa miezi michache tu baada ya kukamilika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti mwaka jana.

Akizungumza katika hafla moja eneo la Siyoi Lonyangapuo alisema kwamba sasa ni wakati ambapo wananchi wanahitaji maendeleo na ni jambo la kusikitisha kwa viongozi kuendeleza siasa badala ya kuhakikisha huduma bora kwa wakazi.

“Inasikitisha kuona kwamba viongozi wameanza kuendeleza maswala ya kisiasa miezi michache tu tangu taifa litoke kwenye msimu wa uchaguzi. Sasa ni wakati ambapo viongozi wanapasa kushirikiana ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi wala si kuendeleza maswala ya siasa.” Alisema Lonyangapuo.

Wakati uo huo Lonyangapuo ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya shirika la maji na maendeleo kaskazini mwa bonde la ufa aliwahakikishia wakazi wa Siyoi kwamba mradi wa maji utakamilika hivi karibuni kabla ya kuzinduliwa rasmi na rais William Ruto ili yaanze kutumika na wakazi.

“Kwa wakazi wa eneo hili la Siyoi nawahakikishia kwamba hivi karibuni mradi wa maji wa Siyoi utakamilika na kuhakikisha kwamba wakazi wanapata maji ya kutosha. Tutakuja huku na rais William Ruto ambaye atazindua rasmi maji haya kabla ya kuanza kutumika.” Alisema.