VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA UKEKETAJI UNAONDELEZWA KISIRI NA BAADHI YA WAZAZI.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia visa vya ukeketaji ambavyo vinaendelezwa kisiri baadhi ya maeneo ya kaunti hiyo licha ya juhudi za viongozi na mashirika mbali mbali ya kijamii kuhakikisha visa hivyo vinakabiliwa.

Wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Kapenguria Richard Mastaluk, viongozi hao walisema kwamba mikakati ambayo imewekwa na serikali pamoja na mashirika mbali mbali kumaliza tamaduni hii iliyopitwa na wakati, imekuwa ikilemazwa na baadhi ya wazazi wanaoiendeleza kisiri.

Mastaluk alisema kwamba tamaduni hii imepelekea kuathirika pakubwa kina mama na watoto wa kike wanaoipitia, ambapo wengi wa watoto wa kike wamekatiziwa ndoto zao kwa kulazimishwa kuolewa punde baada ya kukeketwa.

“Kumekuwepo na visa vya ukeketaji ambavyo vinaendelezwa kisiri na baadhi ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi. Ukeketaji ni tamaduni ambayo imepitwa na wakati. Tumeona jinsi kina mama na watoto wetu wameumia. Mtoto akishakeketwa anatafutiwa mwanamme haijalishi umri wake.” Alisema Mastaluk.

Mastaluk sasa anatoa wito kwa wakazi kujiepusha na tamaduni hiyo na kuwapa nafasi watoto wa kike kusoma na kuafikia ndoto zao maishani jinsi ilivyo kwa wenzao wa kiume.

“Natoa wito kwa wazazi kwamba tuachane na tabia hii ya ukeketaji ili tuwape watoto wetu wa kike nafasi ya kusoma ili wafanane na wenzao wa kiume. Ukeketaji haufai kwa dunia ya sasa na hata Biblia yenyewe inakataa.” Alisema.