VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WALAANI MAUAJI YA MTU MMOJA OMBOLION.
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kukashifu uvamizi wa hivi punde ambao umeshuhudiwa mipakani pa kaunti hii na kaunti jirani ya Turkana ambapo mtu mmoja aliuliwa na wahalifu eneo la Ombolion licha ya oparesheni ya kiusalama ambayo imekuwa ikiendelezwa maeneo haya kwa muda sasa.
Wa hivi punde kuzungumzia swala hili ni spika wa bunge la kaunti ya Pokot magharibi Fredrick Kaptui ambaye alitoa wito kwa serikali kupitia idara ya usalama kutekeleza maswala yaliyojadiliwa baina ya viongozi kaunti hiyo na waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof Kithure Kindiki, ili kutia kikomo kwa mauaji ya wakazi ambayo yameendelea kushuhudiwa.
Aidha Kaptui aliwahimiza wakazi ambao wanaishi maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani za Turkana, Baringo pamoja na Elgeyo marakwet kukumbatia amani ili kuruhusu miradi ya maendeleo kutekelezwa maeneo hayo.
“Nawahimiza wakazi wanaoishi katika mipaka ya kaunti hii na kaunti ya Turkana kwamba tukumbatie amani kwa sababu sasa watu wengi wamepoteza maisha yao kupitia visa hivi vya uvamizi. Natoa wito pia kwa serikali kutekeleza yale ambayo ilijadili na viongozi wa kaunti hii.” Alisema Kaptui.
Kauli yake ilisisitizwa na mwakilishi wadi mteule Mary Cherop ambaye aidha alimtaka waziri Kindiki kuendelea kufanya ziara za kiusalama katika kaunti hizi hadi atakapohakikisha kwamba wavamizi wote wanaosababisha utovu wa usalama wamekabiliwa.
“Namwomba waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kutochoka kuja eneo hili hadi pale usalama utaimarishwa. Naomba pia atuongezee maafisa wa polisi katika maeneo hayo ya mipakani.” Alisema Cherop.