VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WALAANI KUTEKETEZWA MABWENI YA SHULE YA MSINGI YA TARTAR.


Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelaani vikali kisa cha kuteketezwa mabweni mawili katika shule ya msingi ya Tartar.
Wakizungumza baada ya kuzuru shule hiyo viongozi hao wakiongozwa na seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio, aliyekuwa kwa wakati mmoja katibu katika wizara ya elimu Simon Kachapin na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao wamesema kuwa hali hii inadhihirisha uovu katika jamii.
Viongozi hao sasa wamezitaka idara za usalama katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuendesha uchunguzi wa kina na kuhakikisha kuwa wahusika wa tukio hilo wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha wameitaka serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia idara ya majanga kutenga fedha za kuwashughulikia wanafunzi walioathirika katika mkasa huo, wakitaka viongozi pamoja na wadau mbali mbali kushiriki katika juhudi za kuhakikisha shule hiyo inarejea katika hali yake.