VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAKOSOA HATUA YA KUHUSISHWA KAUNTI HII NA UTOVU WA USALAMA.

Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kukosoa dhana kuwa uhalifu mwingi ambao unatokea katika kaunti za bonde la kerio unahusisha jamii ya Pokot.

Wakiongozwa na mbunge wa Kacheliba Titus Lotee, viongozi hao walisema kwamba dhana hii imepelekea kaunti hiyo kushuhudia upungufu wa watu wanaotoa huduma mbali mbali muhimu kwa wananchi kwani wengi wao wanahofia kuhudumu kwenye kaunti hiyo kutokana na dhana hiyo potovu.

“Watu wengi wamesusia kuja kaunti hii ya Pokot magharibi kwa sababu wanasema kwamba ni sehemu ambako kuna utovu wa usalama. Watu wakisikia tu jina Pokot magharibi kinachowajia akilini mwao ni utovu wa usalama hali ambayo imeathiri pakubwa baadhi ya huduma ambazo zinahitaji wataalam kutoka nje ya kaunti hii.” Alisema Lotee.

Viongozi hao walisema kwamba visa vingi vya uhalifu hasa vinavyohusisha wizi wa mifugo hutokea mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani wakidai kwamba madai haya yanaenezwa na watu ambao nia yao ni kuchafua sifa ya kaunti ya Pokot magharibi.

“Hakuna mtu ambaye ameuawa kwa risasi katika kaunti hii kwa miaka kadhaa iliyopita. Maswala ya utovu wa usalama ambao tunasikia ni maeneo ya mipakani. Uvumi huu unaenezwa tu na watu ambao wana nia ya kupaka tope sifa ya kaunti hii.” Alisema.

Wakati uo huo viongozi hao walielezea kuunga mkono oparesheni ya kiusalama ambayo inaendelea katika kaunti sita za kaskazini mwa bonde la ufa ili kuondoa silaha zinazomilikiwa na raia kinyume cha sheria wakisema itapelekea kurejelewa usalama maeneo haya.

“Majirani zetu ndio wanatusumbua. Na ndiyo maana tunataka hii oparesheni ya kuondoa silaha inayomilikiwa kinyume cha sheria  kufanikishwa ili kuhakikisha hali ya utulivu inarejea maeneo husika.” Alisema.