VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAKASHIFU KUTUMWA NYUMBANI WANAFUNZI KILA MARA.


Baadhi ya viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameelezea ghadhabu zao kufuatia hatua ya kutumwa nyumbani baadhi ya wanafunzi katika shule ya upili ya Chewoyet hasa nyakati za jioni kufuatia kutolipa ada ya mitihani.
Wakiongozwa na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu viongozi hao wamesema ni jambo la kusikitisha kwa uongozi wa shule hiyo kuwatuma nyumbani wanafunzi kutafuta fedha hizo hali serikali iliagiza wanafunzi kutozuiwa kufanya mtihani kwa ajili ya fedha hizo wakisema wazazi wanakabiliwa na hali ngumu kwa sasa kutokana na athari za janga la corona.
Kasheusheu amesema kuwa watalazimika kutafuta ufafanuzi kutoka kwa wadau kuhusu swala hili huku akiwataka wakuu wa shule kutowatuma nyumbani wanafunzi kutafuta karo na badala yake kuwasiliana na wazazi wa wanafuzni hao kuhusu jinsi ya kulipa karo.
Ni kisa ambacho pia kimekashifiwa vikali na wazazi mjini makutano ambao wametaka hatua kuchukuliwa dhidi ya uongozi wa shule hiyo.
Hata hivyo mkuu wa shule hiyo amekana madai ya kuwatuma nyumbani wanafunzi hao badala yake akisema kuwa hawajaripoti shuleni tangu kufunguliwa shule, na hata baada ya kuripoti shuleni kwa mara ya kwanza jumapili juma hili, walitoweka tena bila ya ufahamu wa uongozi wa shule hiyo.