VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAKASHIFU KAULI INAYOHUSISHA JAMII YA POKOT NA SHAMBULIZI LA BASI LA SHULE YA TOT.
Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kukashifu hatua ya kuhusishwa jamii ya Pokot na shambulizi la basi la shule ya upili ya Tot kaunti ya Elgeyo Marakwet ambapo dereva wa basi hilo aliuliwa huku wanafunzi 13 na walimu wawili wakijeruhiwa.
Mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ni kiongozi wa hivi punde kukashifu kauli hiyo akisema kuwa waliotekeleza shambulizi hilo ni wahalifu ambao wanafaa kukabiliwa wala si kuihusisha jamii nzima kwa visa kama hivyo.
Moroto amesema kuwa jamii ya Pokot umeishi kwa amani na jamii zingine bila migogoro akidai ni ishara ya utepetevu kwa afisa yeyote wa serikali kuanza kuilaumu jamii moja kwa maswala ya uhalifu.
Wakati uo huo Moroto ameshutumu agizo la waziri wa usalama wa ndani ya nchi Dkt Fred Matiangi la kukamatwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa madai ya kuruhusu basi la shule hiyo kutembea masaa ya kafyu akisema kuwa serikali inafaa kutumia muda wake kuwakabili wahalifu wanaotatiza amani nchini wala si kuweka sheria za kuwakandamiza wananchi.