VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAHUSISHA HATUA YA KUWAHAMI NPR WA UPANDE WA ELGEYO MARAKWET NA MAUAJI YA WATU WAWILI KAMOLOGON.

Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole amesuta hatua ya wizara ya usalama chini ya waziri Kithure Kindiki kuwakabidhi bunduki maafisa wa NPR wanaohudumu upande wa Elgeyo marakwet na kuitenga kaunti hiyo.

Akizungumza alipozuru eneo la Kamologon mpakani pa kaunti hiyo na ile ya Elgeyo Marakwet ambako watu wawili waliuliwa jumatatu wiki hii na majangili, Komole alidai kwamba hatua hiyo imechangia utovu wa usalama kwani inakisiwa bunduki iliyotumika katika mauaji hayo ni ya maafisa wa NPR.

Komole aidha alimtaka rais William Ruto kuzuru eneo hilo ili kutathmini jinsi hali ilivyo hasa katika mipaka ya kaunti ya Pokot magharibi na Elgeyo marakwet, pamoja na Turkana.

“Bunduki ambazo ziko upande wa Elgeyo Marakwet ndizo zimewaumiza hawa vijana. Na tunashuku bunduki hizi ni za maafisa wa NPR. Na haya ndio mambo ambayo tumekuwa tukimlaumu waziri Kindiki kwa kushughulikia swala la utovu wa usalama kwa ubaguzi. Na namwomba rais aje aangalie hali ilivyo maeneo haya ya mipakani.” Alisema Komole.

Kwa upande wake kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam alisema oparesheni ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wakazi itaendelea.

Alitoa wito pia kwa wazee wa kaunti hizi mbili kufanya vikao vya mara kwa mara vya kuangazia hali ya usalama na kuwahimiza vijana kutoka jamii zote mbili kujitenga na visa vya wizi wa mifugo.

“Sasa hivi tunaendeleza oparesheni ya kuondoa silaha haramu mikononi mwa raia. Na oparesheni hii itaendelea hadi silaha zote zitakapotwaliwa. Naomba pia wazee wa jamii zote mbili kufanya vikao vya kila mara na kuwashauri vijana kujitenga na tabia hii ya kuwahangaisha wananchi.” Alisema Katam.