VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUZINGATIA USHIRIKIANO NA KUEPUKA SIASA ZA KILA MARA.


Aliyekuwa mbunge wa Sigor katika kaunti hii ya Pokot Magharibi Philip Rotino ametoa wito kwa viongozi na wakazi wa kaunti hii kudumisha umoja.
Akizungumza na kituo hiki Rotino amewataka viongozi waliochaguliwa kushirikiana na wale ambao hawakufaulu katika uchaguzi mkuu uliopita katika juhudi za kufanikisha huduma kwa wananchi na kujitenga na siasa anazosema kwamba zilikamilika baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.
“Siasa zimeisha na sasa ni wakati ambapo viongozi waliochaguliwa wanafaa kuwahudumia wananchi. Viongozi wote, wale ambao walichaguliwa na wale ambao hatukufanikiwa kuchaguliwa tunapasa kushirikiana katika kuhakikisha kwamba maisha ya wananchi yanaimarika. Sasa si wakati wa majibizano ya kisiasa.” Alisema Rotino.
Aidha licha ya kumpongeza gavana wa kaunti hii Simon Kachapin kwa kuwachagua idadi kubwa ya vijana katika idara bali mbali za serikali yake, Rotino amemtaka pia kuwajumuisha watu wenye uzoefu katika serikali yake.
Amesema kwamba hatua hiyo itawasaidia maafisa katika idara hizo wasio na ujuzi wa kutosha kupata mawaidha kutoka kwa viongozi wenye uzoefu kuimarisha huduma zao.
“Ni vizuri kwamba gavana Kachapin amewachagua vijana wengi katika baraza lake la mawaziri na makatibu. Lakini namsihi aweze kutafuta angalau watu wenye ujuzi hasa wale wenye umri mkubwa ili wasaidie hawa vijana kwa kuwapa ushauri jinsi wanapasa kuendesha shughuli zao.” Alisema.

WhatsApp us