VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAENDELEZA MIKAKATI YA KULETA UTANGAMANO BAINA YA JAMII ZA POKOT NA SEBEI.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameelezea mikakati ambayo wanaendelea kuweka kuhakikisha kwamba jamii za Sebei na Pokot ambazo zimekuwa katika migogoro katika siku za hivi karibuni zinakumbatia amani na kuendeleza shughuli bila ya mivutano.

Wakizungumza wakati wa hafla ya mchango katika kanisa la ELCK eneo la Katikomor, viongozi hao wakiongozwa na naibu gavana wa kaunti hiyo Robert Komole walielezea umuhimu wa kuimarishwa makanisa ya maeneo hayo ambako wakazi kutoka jamii hizo wanakutana katika ibaada kama njia moja ya kuhakikisha kwamba wanatangamana.

“Kama viongozi tunajaribu kuhakikisha kwamba wakazi wa maeneo haya hasa kutoka jamii za Sebei na Pokot wanaishi kwa amani. Na kama njia moja ya kuhakikisha jamii hizi zinatangamana, tunajenga na kuimarisha hali ya makanisa ambayo ni sehemu ambazo wakazi wanakutana.” Walisema.

Kulingana na aliyekuwa gavana kaunti hiyo John Lonyangapuo, suluhu kwa tatizo la usalama maeneo hayo ni kujenga shule akisema  kwamba hatua yake ya kujenga shule za amani maeneo ya mipakani alipokuwa gavana imechangia pakubwa kushuhudiwa amani maeneo hayo baada ya hali ya utovu wa usalama kushuhudiwa kwa miaka mingi.

“Suluhu ya kudumu kwa swala la amani eneo hili na maeneo mengine ya mipakani ni kujenga shule ambazo wanafunzi kutoka jamii zote zinazozozana watakutana na kuendeleza masomo. Nikiwa gavana nilijenga shule hii ya Katikomor na shule zingine na hali hii imechangia pakubwa usalama.” Alisema Lonyangapuo.

Viongozi hao walitoa wito kwa jamii ya pokot kuhakikisha kwamba wanaishi kwa amani na wenzao wa Sebei ili wapate sehemu ya kulisha mifugo yao bila ya mivutano.

“Tunawaomba sana wakazi wa jamii ya Pokot, hata tunapojaribu kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama, wao pia wachangie katika juhudi hizi kwa kuhakikisha kwamba wanaishi na jamii zingine kwa amani ili pia waruhusiwe kulisha mifugo yao na kuendeleza shughuli zingine.” Walisema.