VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WAENDELEA KUPUUZA KUBUNIWA CHAMA KIPYA.


Siku chache tu baada ya mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu kushutumu mipango ya kubuniwa chama kipya katika kaunti hii ya Pokot magharibi, mipango ambayo hata hivyo ilithibitishwa na mbunge wa Pokot kusini David Pkosing, hisia mbali mbali zimeendelea kuibuliwa miongoni mwa viongozi kaunti hii kuhusu chama hicho.
Seneta wa kaunti hii ya pokot magharibi Samwel Poghisio japo amesema kuwa mtu yeyote ana uhuru wa kuanzisha chama, amedai kuwepo mipango ya kutumiwa fedha za umma katika mikakati ya kubuni chama hicho ambacho hata hivyo amesema hakitaafikia lolote.
Aidha poghisio amepuuzilia mbali kuanzishwa chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto katika kaunti hii huku akito wito kwa wakazi kutokuwa wepesi wa kushawishiwa kujiunga na vyama vinavyochipuka na badala yake kusalia katika vyama ambavyo vimekuwepo kwa miaka mingi.
Ni kauli ambayo imetiliwa uzito na katibu katika wizara ya ugatuzi na maeneo kame Mika Powon, ambaye pia ametaja chama hicho kuwa cha kikabila, kisicho na maisha na ambacho hakitoweza kubuni serikali wala hata kujenga upande wa upinzani nchini kwa kuwa kinahusishwa na jamii moja pekee.