VIONGOZI POKOT MAGHARIBI NA ELGEYO MARAKWET WATAKIWA KUCHOCHEA UHUSIANO MWEMA MIONGONI MWA WAKAZI WA KAUNTI HIZO.

Wito umetolewa kwa viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet kuimarisha uhusiano miongoni mwa wakazi wa kaunti hizi mbili kama njia moja ya kukabili uhalifu unaoendelezwa na wezi wa mifugo.

Akizungumza katika ziara yake kaunti ya Pokot magharibi, waziri wa barabara Kipchumba Murkomen alisema kwamba ni jukumu la viongozi katika kaunti hizo mbili kuhakikisha wakazi wanashirikiana katika kuandaa mikutano ya pamoja ya mara kwa mara ili kuwaondoa wahalifu hao.

“Sisi viongozi wa pokot magharibi na Elgeyo marakwet tunapasa kuhakikisha uhusiano mwema wa watu wetu kwa kuandaa mikutano mbali mbali ya pamoja, ili tuweze kuwaondoa wahalifu miongoni mwetu. Sisi ni jamii moja na hatupasi kuuana kiholela.” Alisema Murkomen.

Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wakazi kaunti hiyo kwamba wizara yake inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba kuna barabara bora zitakazoimarisha doria hasa maeneo ambayo yameathiriwa na utovu wa usalama kwa miaka mingi.

“Kwa upande wangu ninafanya juhudi kuhakikisha kwamba kuna barabara bora hasa maeneo ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama ili kuimarisha doria ya maafisa wa polisi maeneo hayo.” Alisema.

Viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na gavana Simon Kachapin walielezea haja ya rais William Ruto kupewa muda wa kutekeleza majukumu yake wakielezea imani kwamba kaunti hiyo na taifa kwa ujumla litaimarika pakubwa chini ya uongozi wake.

“Serikali inaendelea vizuri na ni wakati tunapasa kumpa rais wakati wa kutekeleza majukumu yake. Tuna uhakika kwamba chini ya uongozi wa rais Willima Ruto, kaunti hii na taifa la Kenya litaimarika zaidi.” Walisema.