VIONGOZI MBALIMBALI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WANAZIDI KUTOA WITO WA ADHABU YA VIBOKO KUREJESHWA SHULENI.


NA BENSON ASWANI
Wadau mbali mbali katika sekta ya elimu nchini wameendelea kuunga mkono pendekezo la kurejeshwa adhabu ya kiboko shuleni.
Wa hivi punde kuzungumzia swala hilo ni mbunge wa Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto ambaye amekosoa pakubwa hatua ya kuondolewa adhabu hiyo.
Akizungumza na kituo hiki, Moroto ambaye alikuwa mwalimu kwa wakati mmoja kabla ya kujitosa katika siasa, amesema kuwa nidhamu miongoni mwa wanafunzi imedorora pakubwa kufuatia misururu ya kuteketezwa majengo ya shule hali ambayo imechangiwa na kuondolewa adhabu ya kiboko.
Wakati uo huo Moroto amekosoa katiba ya sasa anayosema inampa haki nyingi mwanafunzi na kumnyima mzazi na mwalimu uwezo wa kumwadhibu mwanafunzi hali ambayo imechangia kudorora nidhamu shuleni.