VIONGOZI KUTOKA BONDE LA KERIO WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA KUKABILI UHALIFU.

Na Benson Aswani
Ipo haja kwa kaunti za Bonde la Kerio ikiwemo kaunti hii ya Pokot magharibi, Elgeyo marakawet na Baringo kushirikiana kwa pamoja katika vita dhidi ya uvamizi ambao umekuwa ukishuhudiwa eneo hili na kugharimu maisha ya wakazi wengi.
Haya ni kwa mujibu wa mbunge wa Sigor kaunti hii ya Pokot magharibi Peter Lochakapong ambaye amesema kuwa uvamizi mipakani mwa kaunti hizi hasa eneo la Chesogon utakabiliwa tu iwapo viongozi katika kaunti hizi watashirikiana kikamilifu kwa nia moja ya kukabili visa hivi.
Wakati uo huo Lochakapong amepongeza hatua ya kubuniwa afisi ya mshirikishi wa kaunti hizi kuhusu swala la usalama eneo la Tot huku akitaka atengewe raslimali za kutosha za kumwezesha kutekeleza kikamilifu shughuli zake.
Hata hivyo lochakapong ameelezea imani ya kukabiliwa uhalifu huu na kushuhudiwa amani maeneo haya kutokana na mikakati ambayo inaendelea kuwekwa huku akiwataka wote ambao wanachochea uovu huo kukoma ili kuwaruhusu wakazi kutekeleza shughuli zao kwa amani.