VIONGOZI KERIO VALLEY WALAUMU SERIKALI KWA KUSHUGHULIKIA UTOVU WA USALAMA KWA UPENDELEO.
Umiliki wa bunduki miongoni mwa baadhi ya wakazi katika bonde la kerio ndicho kikwazo kikubwa katika juhudi za kumaliza uhalifu ambao unaendelea kushuhudiwa eneo hili.
Haya ni kwa kujibu wa aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye aidha amesema kwamba serikali imekuwa ikishughulikia tatizo hili kwa kuegemea upande mmoja kutokana na habari zisizo za kweli ambazo imekuwa ikipokea kuhusu umiliki wa silaha.
“Kikwazo kikuu katika juhudi za kukabili uhalifu katika eneo la bonde la kerio ni umiliki wa bunduki miongoni mwa raia. Raia wengi wa eneo hili wanamiliki bunduki lakini sasa serikali haishughulikii tatizo hili kwa usawa. Inafuata taarifa za kupotosha kwa kuwasikiliza wale ambao wanajitetea kwamba hawana silaha.” Alisema Poghisio.
Aidha Poghisio alilalamikia hatua ya serikali kupitia wizara ya usalama wa ndani ya nchi kuwahami maafisa wa NPR wa upande mmoja kukabili wizi wa mifugo ambao umepelekea maafa ya wakazi wengi na kuyatenga maeneo mengine akitaka kuwepo na usawa katika harakati za kutafuta amani.
“Kosa moja ambalo serikali inafanya ni kufikiria kwamba itawapatia silaha maafisa wa NPR wa upande mmoja na kuacha pande zingine. Serikali inapasa kuwa na usawa katika kushughulikia utovu wa usalama kwa kuwahami maafisa wa NPR wa pande zote iwapo imeamua kuwahami maafisa hao wa akiba.” Alisema.
Wakati uo huo Poghisio alitaja ukosefu wa elimu miongoni mwa wakazi kuwa chanzo cha utovu wa usalama katika bonde la kerio akitaka jamii za eneo hili kukumbatia elimu ambayo ameitaja kuwa suluhu ya pekee kwa tatizo hili.
“Wengi wa raia katika kaunti za bonde la kerio hawajapata elimu na sasa hata hawafahamu kwamba kuna sheria ambayo inakanya dhidi ya kumiliki silaha bila leseni. Elimu inasaidia kubadilisha fikra. Lakini bila elimu hamna chochote ambacho utafahamu kuhusu sheria.” Alisema.