VIONGOZI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WASIKITISHWA NA HATUA YA KUFUNGWA KWA CHUO CHA KISII ENEO LA KERINGET POKOT
Aliyekuwa gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameelezea kusikitishwa na hatua ya kufungwa kwa chuo kikuu cha kisii bewa la Keringet katika kaunti hii.
Akizungumza na kituo hiki Kachapin ambaye chuo hicho kilinzishwa katika utawala wake, amelaumu uongozi wa sasa kwa kile amedai kuwa umekitelekeza chuo hicho kilichonuiwa kuwafaidi wanafunzi kutomka kaunti hii kutokana na sababu za kisiasa.
Aidha kachapin ambaye ametangaza nia ya kuwania tena ugavana wa kaunti hii katika uchaguzi mkuu ujao amesema kuwa alianzisha chuo hicho kwa lengo la kuwanufaisha wakazi wa kaunti hii na kuimarisha uchumi wa kaunti.
Kachapin amesema kuwa wanafunzi wengi katika kaunti hii wataathirika pakubwa kwa kufungwa kwa chuo hicho kwani watalazimika kuhamishwa hadi mabewa mengine ya chuo hicho ambayo yapo nje ya kaunti hii ya Pokot magharibi.