VIONGOZI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAMEHIMIZWA KUDUMISHA AMANI MSIMU HUU WANAPOENDELEZA SIASA ZAO

Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kutoa wito kwa wakazi kuzingatia amani na utulivu hasa wakati huu ambapo siasa za uchaguzi mkuu ujao zimezidi kushika kasi.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha amani inadumu ili kusishuhudiwe ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zimeshuhudiwa katika chaguzi za awali.
Wakati uo huo Moroto amepuuza shinikizo zinazoelekezewa naibu rais William Ruto kumtaka kujiuzulu wadhifa wake baada ya kughura chama cha Jubilee akisema kuwa naibu rais alichaguliwa na wananchi wala si chama.
Kando na hayo Moroto ameshutumu uongozi wa kaunti hii kwa kujihusisha pakubwa na maswala ya siasa na kulitelekeza hospitali ya Kapenguria hali ambayo inawalazimu wanaotafuta huduma za matibabu kuzitafuta nje ya kaunti hii.