VIONGOZI KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAITAKA SERKALI YA KITAIFA KUWACHUKULIA HATUA WALIOHUSIKA NA MAUJI ENEO LA CHESOGON



Katibu katika wizara ya michezo, utamaduni na toradhi za kitaifa Simon Kachapin ameelezea kusikitishwa na utovu wa usalama ambao umeendelea kushuhudiwa mipakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.
Akizungumza na kituo hiki Kachapin ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa kaunti hii amesema kuwa licha ya kuwa wahusika wa visa vya utovu wa usalama wanafahamika na wanajamii, hamna hatua ambazo zimechukuliwa hadi kufikia sasa.
Amezitaka idara za usalama kuchukulia kwa uzito swala hili na kuwasaka wahalifu wanaokaa miongoni mwa jamii ili kuwachukulia hatua na kuhakikisha kuwa hali hii inakabiliwa.
Wakati uo huo Kachapin ametoa wito kwa wakazi kudumisha amani wakati huu ambapo taifa linakaribia uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti huku pia akiwataka wanasiasa kuendesha kampeni zao kwa amani na kutosababisha hali ambayo huenda ikawagawanya wakazi.
Ni wito ambao umekaririwa na seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye amesema kuwa shughuli za kawaida zitarejelewa tu na maendeleo kuafikiwa maeneo haya iwapo wakazi watakumbatia amani.