VIONGOZI BONDE LA KERIO WATAKIWA KUTIA JUHUDI ZAIDI KUHAKIKISHA AMANI INAREJEA ENEO HILO.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kutia juhudi za kuhakikisha kwamba hali ya usalama inadumishwa hasa maeneo ya mipaka ya kaunti hiyo na kaunti jirani za Turkana, Baringo na Elgeyo Marakwet.

Ni wito wake mkewe mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, Mary Moroto ambaye alisema japo kuna juhudi ambazo zinaendelezwa, malengo stahiki hayajaafikiwa katika mchakato mzima wa kuhakikisha wananchi maeneo haya wanaishi kwa amani.

Aidha Bi. Moroto alisema kwamba ni jukumu la viongozi hasa wa kisiasa kuwaelimisha wakazi kuhusu jinsi ya kutunza na kutumia raslimali zinazopatikana kaunti hiyo, ili wajihusishe na shughuli tofauti kando na kutegemea tu kilimo cha ufugaji hali aliyosema itachangia usalama.

“Hawajafanya ya kutosha katika juhudi ambazo wanafanya kuleta amani eneo hili japo yale ambayo wameafikia wamejaribu. Ila sasa waweke juhudi zaidi ikiwemo kuwafunza wakazi umuhimu wa kutunza na kutumia raslimali zinazopatikana kaunti hii. Wasitegemee tu swala la ufugaji ambao ndio chanzo cha uvamizi.” Alisema Bi. Moroto.

Wakati uo huo Bi. Moroto alitumia fursa hiyo kutoa wito wa kujengwa shule maeneo ya mipakani ili kutoa nafasi kwa wakazi kupata elimu.

Alitaka pia viongozi hasa wa kike kuendeleza uhamasisho kuhusu umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike na kubadili mtazamo wa jamii kuhusu mtoto wa kike, kwani pia wana haki ya kupata elimu kwa manufaa yao ya baadaye.

“Shule zijengwe maeneo ya mipakani ili wakazi wa maeneo hayo wasome na kujitenga na maswala ya wizi wa mifugo. Nawahimiza pia viongozi wanawake kuendeleza uhamasisho kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwa manufaa yake ya baadaye.” Alisema.