VIONGOZI BONDE LA KERIO WATAKIWA KUSHIRIKIANA KATIKA JUHUDI ZA KUTAFUTA SULUHU KWA UTOVU WA USALAMA.
Miito imeendelea kutolewa kwa wadau katika kaunti hii ya Pokot magharibi kushirikiana katika kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba amani inadumishwa katika kaunti hii na kaunti zinazopatikana katika bonde la kerio.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni naibu gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Robert Komole ambaye amesema kwamba ili usalama uweze kuimarika katika eneo hili ni lazima wadau wote kutoka pande zote washirikiane kwa kuandaa vikao vya pamoja vya kupanga mikakati ya kuhakikisha hilo linaafikiwa.
Komole aliwasuta hasa viongozi kutoka kaunti hii kwa kutotembea katika njia moja katika kutafuta suluhu kwa utovu wa usalama na badala yake swala hilo kusalia mikononi mwa watu wachache ambao hata hivyo hawaandai vikao vya pamoja kushughulikia hali hiyo.
“Tushirikiane kwa maswala ya amani. Amani ni jukumu letu sote na si la watu fulani. Iwapo kutakuwa na kikao cha kupanga mikakati ya kudumisha amani, viongozi wote katika kaunti hii tunafaa kuwa hapo na kuzungumza kwa lugha moja.” Alisema Komole.
Wakati uo huo Komole alielezea haja ya kutiliwa maanani matakwa ya wananchi hasa wanaoishi maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama ikiwemo kuimarisha barabara za maeneo hayo na kuhakikisha vituo vya polisi vinajengwa.
“Tuwasikilize wananchi. Wana mapendekezo yao ambayo yakizingatiwa huenda ikawa suluhu. Wengi wanataka kuimarishwa hali ya barabara za maeneo husika pamoja na kujengwa kwa kituo cha polisi hasa eneo la Chesogon na maeneo mengine ya mipakani. Tunafaa kuyatilia maanani mapendekezo hayo.” Alisema.