VIONGOZI BONDE LA KERIO WATAKA KUSHIRIKISHA WANANCHI KIKAMILIFU KATIKA KUTAFUTA SULUHU KWA UTOVU WA USALAMA.
Suluhu la utovu wa usalama katika kaunti za eneo la eneo la bonde la kerio liko mikononi mwa wananchi kutoka maeneo hayo.
Haya ni kulingana na aliyekuwa mwaniaji wa ubunge eneo la sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Julius Ariwomoi ambaye alisema kwamba mikakati ambayo inawekwa na serikali pamoja na wadau kukabili hali hiyo imefeli kwa kutokuwa na makini kuhusu jinsi swala hili linafaa kushughulikiwa.
Ariwomoi amesema kwamba wakazi wa maeneo haya wanapasa kushirikishwa kikamilifu katika juhudi za kutafuta amani kwa kuandaa vikao nao ili kuwapa fursa ya kutoa maoni ya jinsi ambavyo swala hili linaweza kushughulikiwa.
“Swala la usalama lina suluhu yake mikononi mwa raia. Wananchi kutoka pande zote ambazo zinakumbwa na uvamizi wa wahalifu wanapasa kuhusishwa kikamilifu katika kutafuta suluhu sio tu kwa serikali kutegemea maafisa wa usalama pekee. Tunapasa kutafuta suluhu kuanzia chini pale mashinani waliko wananchi.” Alisema Ariwomoi.
Wakati uo huo Ariwomoi alitaka wadau wa usalama kuhakikisha kwamba suluhu ya kudumu kwa utovu wa usalama inapatikana kabla ya kurejelewa kikamilifu shughuli za masomo katika shule ambazo zimefungwa maeneo husika.
“Wanafunzi hawapasi kulazimishwa kuingia shuleni maeneo yanayoathirika na utovu wa usalama. Kile ambacho serikali inapasa kufanya ni kutafuta suluhisho la utovu wa usalama kwanza ndipo mikakati ya kuwarejesha wanafunzi shuleni ianze.” Alisema.