VIONGOZI BONDE LA KERIO WATAKA FIDIA KWA WALIOATHIRIKA NA UVAMIZI.

Kama njia moja ya kuponya makovu ya ujambazi katika bonde la kerio, viongozi wa eneo hilo wamesema watapitisha mswada bungeni wa kuwalipa fidia walioathirika na visa vya mara kwa mara vya uwizi wa mifugo katika eneo hilo na maeneo ya baringo.

Wakiongea katika eneo la Arror, Marakwet magharibi viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa marakwet magharibi Timothy Kipchumba wamesifia oparesheni inayoendelea eneo hilo wakiongeza kuwa kwa muda wa miezi sita hakujakuwa na milio ya risasi

“Tumeungana na viongozi wote bungeni kubuni sheria ya kuwepo kwa maafisa wa akiba NPR ili wachunge watu wetu bonde la Kerio. Pia tumeanza kubuni sheria ambayo itahitaji watu wetu ambao wameathirika kutokana na utovu wa usalama Kerio valley wanafidiwa.” Alisema Kipchumba.

Aidha mwakilishi wa kike katika kaunti hiyo Caroline Ngelechei alitaka serikali kukumbuka eneo la bonde la kerio kwa msaada wa chakula kwani hawakuweza kupanda kwa muda wa mwaka moja kufuatia uvamizi wa kila mara.

“kwa sasa sisi hatuna msimu ambao tunavuna. Kwa hivyo tunaomba serikali inapopeana chakula cha msaada kwa kaunti zingine itukumbuke pia sisi.” Alisema Ngelechei.

Naye aliyekuwa mbunge wa marakwet magharibi William Kisang akitaka serikali kufufua ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kama njia moja ya kubadilisha maisha ya wafugaji na kuangazia kilimo cha unyunyuziaji maji mashamba.

“Tumeungana na viongozi wote wa kaunti ya Elgeyo marakwet kuhakikisha kwamba mabwawa ya Kimwarer na Arror yanajengwa ili haya maswala ya uvamizi Kerio valley tuyamalize kwa kufanya kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba.” Alisema Kisang.