Viongozi bonde la kerio washinikiza kuongezwa idadi ya NPR

Titus Lotee – Mbunge wa Kacheliba, Picha/lochele

Na Benson Aswan,

Mbunge wa Kacheliba kaunti ya Pokot magharibi Titus Lotee amesema pana haja ya serikali kufanikisha mipango itakayohakikisha maeneo ya kiutawala mipakani mwa kaunti ya Pokot Magharibi na jirani zake, yanatumika kwa faida ya wananchi.

Akiongea jumatatu katika eneo la Tapach, lotee alitaka idadi ya maafisa wa polisi wa akiba NPR kuongezwa na kufanikisha ujenzi wa kambi, ili kuwapa mazingira bora ya kutoa ulinzi kwa umma.
Alisema hatua hii itasaidia kuhakikisha kwamba visa vya uhalifu vinavyoshuhudiwa maeneo hayo vinakabiliwa.


“Maafisa wa usalama ni wachache zaidi maeneo ya Nauyapong na Ombolion. Kile tunaomba ni kwa waziri wa usalama kuhakikisha kwamba maafisa zaidi wanaajiriwa na kujengewa kambi,” alisema Lotee.


Naye mwenyekiti wa bodi ya maji kaskazini mwa bonde la ufa Prof. John Lonyangapuo, alisema changamoto ya uhaba wa maji kwenye jamii za wafugaji imesuluhishwa kwa kiwango kikubwa.


Aliongeza kwamba serikali kupitia idara hiyo inalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa maji katika maeneo ya wafugaji ambao wamekuwa wakihamahama hadi kaunti nyingine kutafuta bidhaa hiyo muhimu.


“Tuliona kwamba inawezekana kutumia maji kuleta amani katika kaunti hizi, na ndipo tulikuja na mradi wa ‘water for peace’ ili kuunganisha kaunti za bonde la Kerio. Ingawa bado tunashuhudiwa visa hapa na pale ila tunaweza sema mradi huu umesaidia kupunguza pakubwa visa hivi,” alisema Lonyangapuo.


Uhaba wa maji na lishe ya mifugo miongoni mwa jamii za wafugaji ni miongoni mwa sababu ambazo zimetajwa kuchangia pakubwa mizozo ambayo imekuwa ikishuhudiwa kwa miaka mingi eneo la Bonde la Kerio.