Viongozi bonde la Kerio wakabana koo kuhusu utendakazi wa Murkomen

Samwel Moroto mbunge wa Kapenguria,Picha/Maktaba
Emmanuel Oyasi,
Baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamemtetea waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Kipchumba murkomen dhidi ya shutuma kutoka kwa baadhi ya viongozi kuhusu utendakazi wake.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao walimsuta hasa mbunge wa Baringo kaskazini Joseph Makilap ambaye alimtaka waziri Murkomen kupigwa kalamu kwa madai ya kushindwa kuangazia swala la utovu wa usalama eneo hilo.
Viongozi hao walimtaka Makilap kukoma kuingilia utendakazi wa waziri Murkomen hasa anapochukua hatua dhidi ya viongozi katika idara ya usalama ambao wamekuwa wakifanikisha visa vya uvamizi katika kaunti za bonde la Kerio.
“Tunapoona viongozi wenzetu wakitoa matamshi ya kumkashifu waziri wa usalama tunasikitika sana kwa sababu hii ni kuwachochea wananchi,” alisema Moroto.
Wakati uo huo mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alimtaka waziri Murkomen kushughulikia swala la uchimbaji madini haramu, ambao unaendelea katika kaunti ya Pokot magharibi, akidai kwamba wapo baadhi ya maafisa wa serikali wanaowalinda wachimbaji madini hao.
“Nataka kumhimiza waziri Murkomen kwamba ana jukumu la kushughulikia swala la uchimbaji madini haramu katika kaunti hii, kwa sababu wapo baadhi ya maafisa wakuu serikalini ambao wanalinda watu hawa,” alisema Lochakapong.
Akizungumza na wanahabari nje ya hospitali ya rufaa ya kaunti mjini kabarnet, mbunge wa Baringo kaskazini Joseph Makilap ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wengine kaunti hiyo alimsuta waziri Murkomen kwa madai ya kushindwa kuangazia swala la utovu wa usalama hasa katika wadi ya Bartabwa na Saimo Soi.
Makilap alisema uvamizi wa ijumaa juma lililopita katika eneo la chemoe ambapo watu wawili waliuawa na takriban sita kujeruhiwa ulitokana na utepetevu wa waziri huyo.
“Umma kwa sasa hauna imani na utendazi wa Murkomen katika wizara ya usalama wa ndani ya nchi. Rais william Ruto anastahili kuchukua hatua na kumfuta kazi Murkomen kwa sababu ameshindwa kuhakikisha kuna usalama na sasa anatishia jamii,” alisema Makilap
Kiongozi huyo pia alitaka kuhamishwa kwa wakuu wa usalama kwenye kaunti ya Baringo akiwamo kamishna Stephen Kutwa akisema wameshindwa kuwahakikishia wakazi usalama.