VIONGOZI BONDE LA KERIO WAENDELEA KULAANI MAUAJI YA WANAFUNZI WAWILI KAUNTI YA ELGEYO MARAKWET.


Siku kadhaa baada ya majangili waliojihami kwa bunduki kuwauwa kwa risasi wanafunzi wawili katika kaunti ya Elgeiyo marakwet, mbunge wa Tiaty katika kaunti ya Baringo William Kamket ameongoza mkutano wa pamoja wa amani unaolenga kusaka suluhu kwa swala la wizi wa mifugo.
Akiongea katika mkutano huo ulioandaliwa kwenye eneo la Kositei kamket alilaani mauaji ya wanafunzi hao wasichana huku akiyataja kama ishara ya uoga na kipumbavu, ikizingatiwa kwamba hawakuwa wamejihami kwa silaha yoyote.
Kamket aliongeza kuwa tayari wana majina ya watu wanaoshukiwa kuhusika katika shambulizi hilo na kwa sasa viongozi wa nyumba kumi, wale wa kijamii na vijana wanaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wanatiwa nguvuni  na mifugo walioibiwa kurejeshwa.
Aidha Kamket alipongeza utulivu ambao umekuwapo kwa miezi kadhaa sasa huku pia akizihimiza jamii zote za eneo la bonde la kerio kuendelea kuishi kwa amani na kutokubali wahalifu wachache kuchochea uhasama bina yao.
“Wale vijana wajinga ambao walienda kuua wanafunzi kule marakwet ninafurahi kwa sababu majina yao yako na polisi na wazee wa nyumba kumi. Hawa vijana wanafaa kutafutwa na kukamatwa na kuchukuliwa hatua. Sisi hatukubali maswala ya kijinga ya kuua watoto wa wenyewe.” Alisema Kamket.
Kwa upande wao viongozi wa kijamii wakiongozwa na Paul Lotudo walisema kuwa kila mshukiwa wa wizi wa mifugo atawajibishwa pekee yake na kwamba hawatakubali watu wachache kuendelea kupaka tope jamii ya eneo hilo.
“Tunashutumu vikali kitendo hicho na tunaomba hawa wakora wakamatwe ili amani irejee na tuishi na jamii ya marakwet kwa njia inayofaa. Kila mtu abebe mzigo wake iwapo atapatikana kuhusika uhalifu na wasijumuishe jamii nzima katika uhalifu huo.” Alisema Lotudo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi eneo hilo, wale wa kijamii, maafisa wa utawala wakiwamo machifu na manaibu wao pamoja na zaidi ya wafugaji 500 ambao wameahidi kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kunakuwapo na amani ya kudumu.