VIONGOZI BARINGO WAENDELEA KUMWOMBOLEZA NAIBU GAVANA.

Viongozi mbalimbali kwenye kaunti ya Baringo wameendelea kumwomboleza naibu gavana kaunti hiyo Charles Kipng’ok aliyefariki dunia jumatano jioni kwenye uwanja wa ndege wa jomo kenyatta jijini Nairobi.

Wakiongozwa na aliyekuwa gavana wa pili Stanley Kiptis wamemtaja marehemu Kipng’ok kama mtu mkarimu na aliyekuwa tayari kuwahudumia wananchi kutokana na bidiii yake.

Wakiongea baada ya kuzuru nyumbani kwake katika eneo la solian aidha viongozi hao wamemtaja kipng’ok kama mtu aliyekuwa na moyo wa kuwasaidia watu wenye mahitaji katika jamii.

Pia wafanyakazi wa kaunti wakiongozwa na kaimu katibu wa kaunti Elijah Kipkoros wamesema kuwa kifo cha Kipng’ok ni pigo kwa kaunti hiyo huku pia wakiwarai wakazi na wakenya kuiombea familia yake.

Yanaarifiwa haya huku Kamati kadhaa zikibuniwa kwa ajili ya kufanikisha maandalizi ya mazishi ya naibu gavana huyo wa kaunti hii ya Baringo.

 Gavana kaunti hiyo Benjamin Cheboi amesema kuwa kamati moja itakuwa ile ya familia ya mwenda zake na nyingine itakayowashirikisha maafisa wa serikali ya kaunti.

 Kwenye kikao na wanahabari gavana Cheboi amesema kwamba kamati hizo mbili zitashirikiana kwa karibu katika maandalizi na mipango ya mazishi ya merehemu kipng’ok.

Kulingana na taarifa kipng’ok alipatwa na matatizo ya kupumua alipokuwa akijiandaa kusafiri kuelekea jijini mombasa kuhudhuria kongamano la magavana.