Vikao vya kuwahamasisha wakazi dhidi ya ndoa za mapema vyaendelezwa Pokot magharibi

Masika Mwinyi afisa wa miradi katika shirika Youth for a Sustainable World YSW, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Shirika la Youth for a Sustainable World YSW linaendeleza uhamasisho maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi katika juhudi za kukabili visa vya ukeketaji na ndoa za mapema na pia mimba za utotoni.
Akizungumza baada ya kikao na wadau mbali mbali katika mkahawa mmoja mjini Makutano, afisa wa miradi katika shirika hilo Masika Mwinyi alisema lengo kuu la vikao hivyo ni kuhakikisha kwamba haki za watoto zinalindwa na pia kuhakikisha wazazi wanafahamu umuhimu wa watoto wao kwenda shule.
“Tumekuja pamoja na wadau wengine kuwahamasisha wakazi kaunti hii kuhusu haki za watoto pamoja na kusisitiza umuhimu wa wazazi kuwapeleka wanao shuleni,” alisema Mwinyi
Kulingana na meneja wa Kenya Big Dream katika shirika la World Vision anayesimamia kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Baringo Mokita David, kaunti hizo mbili ni miongoni mwa kaunti ambazo zinaongoza katika visa hivi, na hatua hii itasaidia katika kuvipunguza.
“Tukiangalia takwimu, kaunti ya Pokot magharibi na Baringo zipo miongoni mwa kaunti ambazo zinaongoza kwa maswala ya ndoa za mapema, na kupitia vikao hivi tutahakikisha kwamba hali hii inashughulikiwa,” alisema Mokita.
Afisa wa huduma za watoto eneo bunge la Kapenguria Wilfred Azegele alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kushirikiana na maafisa hao katika kuendeleza shughuli hiyo na pia kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa hasa wakati huu ambapo wapo nyumbani kwenye likizo.
“Nawasihi wakazi wa kaunti hii kushirikiana na maafisa hawa wanapoendeleza shughuli ambazo zimepangiliwa. Na pia nawahimiza wazazi kuwalinda vyema wanao msimu huu ambapo wapo nyumbani kwa likizo ya mwezi Aprili,” alisema Azegele.