VIJANA ZAIDI WANUFAIKA NA HUDUMA ZA PENDO AFRIKA POKOT MAGHARIBI.


Idadi kubwa ya vijana katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamenufaika pakubwa kutokana na huduma za kiutu zinazotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Pendo Afrika.
Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo Faith Tanui, Pendo Afrika linashughulika zaidi na kuwashauri vijana kuhusiana na maswala ya elimu, mimba na ndoa za mapema, ushauri dhidi ya matumizi ya mihadarati ambapo kufikia sasa zaidi ya watoto 60 wa kike wamepokea mafunzo kuhusu mimba na ndoa za mapema huku zaidi ya vijana 40 wa kiume wakisaidika dhidi ya matumizi ya mihadarati.
Hata hivyo Tanui amesema kuwa ni vijana wa kike ambao wamekumbatia huduma zao kikamilifu ikilinganishwa na wenzao wa kiume akiwahimiza kujitokeza kwa wingi kukumbatia huduma hizo kwani zitawafaa zaidi maishani.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na Hellen Ngaruiya ambaye ni mshauri nasaha katika shirika hilo na ambaye pia ameitaka jamii katika kaunti hii kukumbatia ushauri nasaha ili kupunguza visa vya watu kujitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo au utumizi wa mihadarati.