VIJANA WAHIMIZWA KUKUMBATIA KOZI ZA UHANDISI.
Wito umetolewa kwa vijana wa kike kujitokeza kwa wingi na kusomea kozi za uhandisi na kupuuzilia mbali dhana ya kuwa baadhi ya taaluma na kazi ni za vijana wa kiume pekee.
Hayo ni kwa mujibu wa msiamizi mkuu wa chuo cha Kitaifa cha Kitale national polytechnic John Otieno Akollah akisema kuwa taaluma ya uhandisi inatoa nafasi kubwa ya kujiajiri na utoaji wa nafasi za kazi kwa vijana.
“Tunatilia mkazo katika kutoa mafunzo kwa vijana wa kike katika kozi za uhandisi. Tunataka kuwawezesha vijana wa kike.” Alisema.
Aliongeza kuwa, “Tunawahimiza vijana wa kike kujitokeza kwa wingi. Wasihofu kuchukua kozi hizi kwa madai kuwa zimetawaliwa na wenzao wa kiume kwa sababu zitawawezesha kujitegemea siku za usoni.”
Wakati uo huo Akollah alisema chuo hicho kimeanzisha mpango mwafaka wa utoaji wa mafunzo ya kiufundi kwa wanafunzi wake kwa jina Work study program ambapo wanafunzi wanapata nafasi ya kusoma na kujifunza kupitia kwa utoaji wa huduma kwa baadhi ya miradi ya maendeleo chuoni humo.
“Katika chuo hiki hatuwafunzi tu wanafunzi bali tunawekeza maarifa kwao. Kwa mfano tunawatumia wanafunzi kutekeleza baadhi ya miradi katika chuo hiki ili wawe katika nafasi ya kufanya kazi wakati wanapoendelea na masomo yao.” Alisema.