VIJANA TRANS NZOIA WATAKA KUFANYIWA MAREKEBISHO SHERIA ZA UCHAGUZI.


Ipo haja ya wabunge kutathmini upya na kufanyia marekebisho sheria zinazo husiana na uchaguzi kufuatia tetesi zinazoibuliwa na wale wasioridhishwa na matokeo ya chaguzi hizo.
Wakizungumza katika Gereza kuu la Kitale baada ya kuachiliwa huru kwa Alpha Chore aliyewasilisha kesi ya kupinga uchaguzi wa Gavana Patrick Khaemba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017, vijana Kaunti ya Trans-Nzoia wamesema kwamba faini zinazotolewa kwa wanaowasilisha kesi za kupinga chaguzi hizo ni za juu zaidi, na itakuwa vigumu kwa wale walio na malalamishi kuwasilisha lalama hizo mahakamani.
Aidha Vijana hao wamesema wanahofia ikiwa marekebisho hayo hayatafanyika uchaguzi ujao huenda usiwe wa kidemokrasia na pia kuwanyima nafasi ya kikatiba ya kuwasilisha malalamishi yao kupitia kwa mahakama kutokana na faini hizo za juu.
Chore ameachiliwa huru baada Maurice Bisau kumsaidia kulipa kiasi cha pesa kisichojulikana baada ya mahakama ya Kitale kumuamuru kugharamia kesi hiyo kwa kulipa shilingi Milioni 11 kwa Gavana Patrick Khaemba na tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.