VIJANA TRANS NZOIA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA VYUO VYA KIUFUNDI.


Wanafunzi 132 kutoka vyuo vya anuwai vya Machungwa, Rafiki na Kitale wamefaidi msaada wa vifaa vya kiufundi kupitia ushirikiano wa wizara ya Elimu Kaunti ya Trans-Nzoia na shirika la Child Rescue Kenya.
Kwenye mkao na wanahabari, msimamizi mkuu wa shirika hilo Stephen Baraza amesema wamechukua hatua hiyo ili kuhakikisha vijana wanaofuzu kutoka kwa vyuo hivyo wanapata nafasi ya kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea kuajiriwa, akitoa wito kwa vijana zaidi kujiunga na vyuo hivyo akisema nafasi kubwa ya ajira kwa sasa ipo katika Elimu ya kiufundi.
Ni matamshi yaliyoungwa mkono na afisa mkuu wa wizara ya Elimu Kaunti ya Trans-Nzoia Susan Ngera, akisema Kaunti ya Trans-Nzoia imejenga zaidi ya vyuo anuwai 31 na ina jumla ya wanafunzi 3000, akitoa wito wa ushirikiano zaidi kutoka kwa wahisani ili kuhakikisha maisha ya usoni ya wanafunzi kutoka vyuo hivyo inaafikiwa, akiongeza kuwa wizara yake inanuia kuajiri walimu zaidi katika vyuo hivyo vya anuwai.