VIJANA 7 KUTOKA POKOT MAGHARIBI WAZUILIWA KATIKA KITUO CHA POLISI CHA LOKICHAR, TURKANA.


Viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi wametoa wito wa kuachiliwa huru vijana saba ambao wanadaiwa kushikiliwa katika kituo cha polisi cha Lokichar katika kaunti ya Turkana baada ya kukamatwa eneo la Kainuk mpakani pa kaunti hizi mbili.
Awali viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Pokot kusini David Pkosing walishutumu vikali kutoweka vijana hao kwa njia isiyoeleweka wakidai huenda walitekwa nyara na watu wasiojulikana, wakielezea hofu huenda kisa hiki kingetokea kama kilichotokea miaka mitatu iliyopita ambapo vijana kutoka kaunti hiyo walitekwa nyara na kisha kupatikana katika msitu mmoja kaunti ya uasin Gishu wakiwa wameuawa.
“Ng’ombe waliuawa tarehe mbili, na tarehe tatu wakati ambapo watoto wanaochunga ng’ombe wamerejea nyumbani, Sisi kama viongozi wa eneo hili tukaona vijana saba wamepotea. Kwa hivyo tusema huenda vijana hao wametekwa nyara na wahalifu.” Alisema Pkosing.
Hata hivyo muda mfupi baadaye Pkosing alituma ujumbe kwenye mtandao wake wa twitter akiwahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kwamba vijana hao wako salama katika kituo cha polisi cha Lokichar baada ya kuhakikishiwa na kamanda wa polisi kaunti ya Turkana.
“Nimezungumza na kamishna wa eneo la rift valley Bw. Hassan na kamanda wa polisi, Bw. Ndanyi ambao wamenihakikishia kwamba vijana hao wako salama mikononi mwa polisi.” Ilisema nukuu ya Pkosing.
Pkosing aliwataka wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi kuendelea kuwa watulivu na kudumisha amani na kutolipiza kisasi wakati ambapo viongozi wa kaunti hiyo wanaendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto hii.
“Nawaomba wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kusalia watulivu na kudumisha amani wakati huu ambapo sisi kama viongozi wa pokot magharibi tunaendeleza mikakati ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo hili.” Alisema.
Kulingana na OCPD wa Turkana kusini William Adenyo vijana hao walikamatwa baada ya kulishambulia gari lililokuwa likisafirisha abiria kuelekea lodwar eneo la turkwel.